Mabadiliko ya Tabianchi na Nafasi ya Mwananchi Katika Kukabiliana na Kustahimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi

Moja ya ajenda kubwa zilizopo katika uga wa kimataifa na zinazogusa uhai wa dunia na viumbe vilivyomo akiwemo mwanadamu ni mabadiliko ya tabianchi.

 

Ndio maana nchi nyingi duniani zimekuwa zikishiriki katika mikutano ngazi ya kimataifa kujadili masuala ya mabadiliko ya tabianchi na kusaini mikataba mbalimbali ikiwa ni pamoja na Agano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) liliopitishwa mwaka 1992 kwa lengo la mwisho la kuzuia wanaadamu kuathirika na hatari ya mfumo wa hali ya hewa. Itifaki ya Kyoto ya 1997 (Kyoto Protocol) na Makubaliano ya Paris ya 2015 ni sehemu ya matokeo ya Agano hili la Kimataifa la UNFCCC.

Makubaliano haya yamelenga kupunguza kiwango cha joto duniani hadi chini ya nyuzi mbili, kwa kupunguza gesi ya Carbon au ukaa inayotoka viwandani.

Aidha, Makubaliano haya ya Paris yanatambua uwezekano wa kuathiriwa kwa nchi zote kwa madhara ya mabadiliko ya tabianchi na kutoa wito wa juhudi maalumu za kupunguza madhara, hasa katika nchi zinazoendelea ambazo hazina rasilimali za kufanya hivyo peke yao ikiwemo nchi ya Tanzania.

 

Pamoja na kwamba mabadiliko ya tabianchi huathiri karibu sekta zote kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, maji, misitu na nyinginezo, shughuli za kibinadamu zina mchango mkubwa katika suala hili.

Tanzania kama ilivyo katika maeneo mengine duniani, tayari imeanza kushuhudia mabadiliko ya tabianchi na moja ya maeneo yaliyokumbwa na janga hilo ni Safu za Milima ya Lyamba la Mfipa na Ziwa Rukwa katika Mkoa wa Rukwa.

 

Kwa mujibu wa Mshauri wa Maliasili na Mazingira Mkoa wa Rukwa, Ndugu Nicolaus Mchome, Safu za milima ya Lyamba la Mfipa ina baioanuai inayohusisha wanyamapori na viumbe wengine, pamoja na kuwa ni vyanzo vya maji kwa wakazi waishio pembezoni mwa Safu hizo na ni sehemu ya uhai wa Ziwa Rukwa.

 

Anaeleza kwamba wanyama wanaopatikana huko ni pamoja na wale wanaotambaa, mbega wekundu katika misitu ya Mbuzi na Mbizi, pia ngedere, fisi, nyani, kima, nguruwe, na ndege wa aina mbalimbali.

 

Ndugu Mchome anaeleza kwamba kumekuwapo na uharibifu mkubwa wa mazingira ya Safu za Milima ya Lyamba lya Mfipa kutokana na kushamiri kwa shughuli za kibinadamu zikiwemo uwindaji [haramu] wa wanyamapori, ukataji na uchomaji moto misitu, kilimo kando ya vyanzo vya maji na ufugaji.

 

Zipi athari za uharibifu huo wa mazingira?

 

Afisa Programu wa Lawyers' Environmental Action Team (LEAT) Ndugu Franklin Masika anaeleza kwamba uharibifu huo unahatarisha uhai na uwepo wa Ziwa Rukwa.

 

Ndugu Masika anasema athari hizo tayari zimeanza kuonekana moja kwa moja ndani ya Ziwa Rukwa, ambapo kina cha ziwa hilo kinapungua kadri siku zinavyokwenda kutokana na mlundikano wa tope linalotokana na mmomonyoko kwenye milima ya Lyamba lya Mfipa na vyanzo vingine vya maji vinavyotiririsha maji kuelekea Ziwa Rukwa. Kutokana na hali hiyo, upo uwezekano unaotishia kuharibika na kutoweka kwa ziwa hilo na rasilimali zake.

 

Pia, kuathirika kwa kilimo kinachotegemea mvua kutokana na kukauka kwa mito iliyopo, kuharibika kwa miundombinu kutokana na mafuriko, kwani maji hayatakuwa na vizuizi hasa kipindi cha mvua, pamoja na mazao kusombwa na maji wakati wa msimu wa mafuriko.

 

Anasema kwamba uharibifu wa safu za milima ya Lyamba lya Mfipa pia unasababisha kupotea kwa baadhi ya viumbe hai wanaotegemea maeneo hayo kama makazi yao kwa mfano, mbega wekundu katika Msitu wa Mbuzi uliopo wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.

 

Nini kinafanyika kudhibiti uharibifu huo wa mazingira?

 

Kutokana na hali hiyo LEAT kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira, Taasisi ya Maendeleo Endelevu Rukwa (RUSUDEO), halmashauri za wilaya za Sumbawanga na Nkasi kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa inatekeleza mradi wa miaka mitano (Machi 6, 2020 hadi Machi 5, 2021) uitwao Usimamizi Endelevu wa Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID). Mradi huu unatekelezwa katika vijiji 15 yaani vijiji vinane katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na saba wilaya ya Nkasi.

 

Msimamizi Mkuu wa Mradi huo, Bi Hana Lupembe anaeleza kuwa malengo ya mradi ni kuwajengea uwezo wananchi kuzifahamu na kuzisimamia rasilimali zinazowazunguka ili kuweza kuzitunza, kufahamu majukumu yao katika kuzuia uharibifu wazo na kuweza kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Aliendelea kusema kuwa Mradi huo utawawezesha wananchi na serikali za vijiji kuweza kutunga na kusimamia sheria ndogo za maliasili zao.

 

Aidha, mradi unawezesha wananchi kujengewa uwezo wa kuhoji juu ya matumizi, ufikiaji na ufanyaji wa maamuzi juu ya rasilimali zao, utumiaji wa fursa ya kupata taarifa juu ya mapato na matumizi ya maliasili zao kupitia nyanja tofauti tofauti ikiwemo mikutano ya vijiji.

 

"Tumekuwa tukitoa elimu kwa makundi mbalimbali kama vile halmashauri za vijiji na kamati zilizoundwa kusimamia maliasili zao ngazi za vijiji ambazo ni kamati za maji, ardhi, mazingira za vijiji na mabaraza ya usuluhishi ngazi za kata. Makundi yote yanawezeshwa kufahamu taratibu na kanuni sahihi za usimamiaji wa maliasili zao na sheria za kimataifa na kitaifa zilizotungwa na bunge kuwezesha utumiaji endelevu wa maliasili zao" alisema Bi Lupembe.  

 

Bi Lupembe, anasema pia kundi la wananchi ambao wanapewa mafunzo ya usimamizi wa maliasili na Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii (UUJ) kama dhana inayowasaidia kuweza kusimamia na kulinda rasilimali zao za asili zinazowazunguka.

 

Matokeo Chanya yaanza kuonekana!

 

Baada ya wananchi na kamati mbalimbali za usimamizi wa maliasili na mazingira za vijiji kupatiwa elimu ya uhifadhi wa mazingira na maliasili, vijiji vya Kisula na Malongwe vilivyopo wilayani Nkasi vimeweza kutunga sheria ndogo nane zinazolenga kusimamia misitu, ardhi, maji na wanyamapori.

 

Mtendaji wa Kijiji cha Kisula, Alexander Joseph Kibelenge amesema kwa kuwa shughuli za kibinadamu ndio changamoto kubwa ya usimamizi wa mazingira na ulinzi wa rasilimali zao hivyo kwa kuzingatia wameona umuhimu wa kutunga sheria hizo.

 

"Tumehamasishwa na LEAT na Mwanasheria wa Halmashauri yetu ya Nkasi kutengeneza sheria hizo kadri ya matakwa ya Katiba ya Nchi ambayo inayowataja wananchi kuwa wasimamizi, watengeneza sera, watunga sheria za kusimamia rasilimali zao" anasema Ndugu Kibelenge.

 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nkasi, Ndugu Kwangura Missana anasema sheria hizo zinasubiri baraka za vikao vya Baraza la Madiwanikupitishwa kisha zitasainiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nkasi kisha zitapelekwa kwenye vijiji husika. Huko nako Mtendaji wa Kijiji na Mwenyekiti wa Kijiji watasaini ndipo zitaanza kutumika, ambapo zitasaidia sana kudhibiti uharibifu wa mazingira katika maeneo ya vijiji hivyo vinavyopitiwa na Safu za Milima ya Lyamba lya Mfipa.

 

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira ya Kijiji cha Kisula, Ndugu Regina Chakupewa anaeleza kwamba sheria hizo zitasaidia sana kudhibiti shughuli zote haramu za kibinadamu ndani ya safu za milima ya Lyamba lya Mfipa. Pia, itaokoa bayoanuai inayohusisha viumbe na wanyama wengine walioanza kupotea.

 

Ni matarajio yetu kwamba wakati elimu ya usimamizi endelevu wa maliasili ikiendelea kutolewa kwa wananchi, huku wakipatiwa njia mbadala za kupata vipato, kufanyika kwa mipango wa matumizi bora ya ardhi, utungwaji wa sheria ndogo zinazotarajiwa kutungwa katika vijiji vyote 15 vya mradi, itakuwa ni chachu ya kupunguza matumizi yasiyo dumivu ya maliasili kwa kuwa wataongeza jitihada za utunzaji wa rasilimali hizo, na hivyo kupunguza athari za mabadiliiko ya tabianchi”, alimalizia Dada Hana Lupembe.

0
0
0

Our   Partners