Usimamizi Endelevu wa Maliasili ni Mradi mtambuka wa miaka mitano (2020-2025) unaolenga kuimarisha Usimamizi Endelevu wa Maliasili Mkoani Rukwa katika Wilaya za Sumbawanga na Nkasi. Mradi huu unafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Watu wa Marekani. Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Maliasili unaotekelezwa na Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo Endelevu yaani RUSUDEO unatambua utajiri wa Rukwa. Kimahususi kabisa mradi unatambua uwepo na umuhimu wa rasilimali za Maliasili zinazopatikana katika milima ya Lyamba lya Mfipa.

Utajiri wa eneo hili ulithibitishwa na LEAT na RUSUDEO kupitia utambulishaji na tathimini ya mradi iliyofanyika kati ya tarehe 13-06-2020 hadi tarehe 24-06-2020. Ukusanyaji wa taarifa katika tarafa za Chala, Kate na Mtowisa, kata za Nkandasi, Mkwamba, Kipande, Muze, Kalumbaleza na mwadui na vijiji 15 vya mradi ulitosha kudhihirisha ukubwa, umuhimu na hali za usimamizi wa maji, misitu, wanyamapori na ardhi. Itoshe kusema wakazi waishio sambamba na milima na misitu ya Lyamba lya Mfipa hutegemea maliasili kukidhi mahitaji yao ya kimaisha. Maji ni muhimu nyumbani, kwa kilimo na unyweshaji wa mifugo. Ardhi ni msingi mkuu wa shughuli za kiuchumi kwa jamii kwani hutoa fursa kwa wakazi kuendesha kilimo na ufugaji. Kadhalika, bayoanuai huboresha uwiano wa ki-ikolojia.

Pamoja na faida lukuki za ardhi, misitu, wanyamapori na maji bado usimamizi wa rasilimali hizi unazungukwa na changamoto nyingi hivyo kufifisha fursa za wananchi na ustawi wa rasilimali. Vyanzo vya maji, kwa mfano, vinaendelea kuvamiwa na shughuli za kilimo na ufugaji, ongezeko la sumu na vimelea vya magonjwa na mmong’onyoko wa udongo. Kuvunjika kwa madaraja tarafa ya Mtowisa ni kielelezo tosha cha namna Mabadiliko ya Tabianchi na uvunaji usiofuata taratibu ulivyo mbaya kwa ustawi wa watu na ulinzi wa mali zao. Kama vile haitoshi, wakazi wa vijiji hususani ukanda wa chini wa Lyamba lya Mfipa hushambuliwa na maradhi ya matumbo kutokana na kuchafuliwa kwa vyanzo vya maji.

Ni kwa muktadha huu LEAT na mshirika wake RUSUDEO wameadhimisha mkutano wa uzinduzi na tathimini ya mradi mnamo tarehe 5-08-2020 ili kutekeleza mradi huu wa Usimamizi Endelevu wa Maliasili kama mkakati wa kuelekea katika usimamizi thabiti wa rasilimali za maliasili. LEAT na RUSUDEO tunaamini uwazi, uwajibikaji, utawala wa sheria na ushiriki wa wananchi katika kutunza rasilimali ni mwanzo wa kuongeza ustahimilivu wa jamii. Timu ya utekelezaji wa mradi inaamini ili kufikia utawala bora wa maliasili lazima jamii iwezeshwe ki-ufahamu na ki-zana (tools). Hivyo elimu kwa wadau, kusaidia kutengeneza mipango ya matumizi ya ardhi, kusaidia kuboresha uelewa na ufahamu wa kamati mbalimbali, kuratibu utengenezwaji wa sheria ndogo, upandaji miti, kufanya kazi na vikundi vya kijasiriamali ni jitihada ya kuelekea katika jamii yenye usimamizi madhubuti wa maliasili kwa kuzingatia upatikanaji wa haki za msingi za binadamu na viumbe.

Kupitia mkutano wa uzinduzi wa mradi, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa, Tanzania (USAID Tanzania), Ndugu Andy Karas, alitoa Salamu za Uzinduzi wa mradi wa Usimamizi Endelevu wa Maliasili kwa LEAT na mruzuku wake pamoja viongozi na wadau wa mradi kutoka ofisi ya mkoa wa Rukwa, halmashauri za Nkasi na Sumbawanga, Tarafa, Kata na vijiji vya mradi. Moja ya jambo alilosisitiza kufanyika kupitia mradi huu ni kuimarisha uwezo wa mamlaka za serikali za vijiji na upangaji wa matumizi ya ardhi ili kupunguza uharibifu wa vyanzo vya maji na kuongeza uhifadhi wa misitu na wanyamapori katika safu za milima ya Lyamba lya Mfipa.

Bonyeza hapa kusikiliza salamu za uzinduzi wa mradi kutoka kwa Mkurugenzi Mkazi wa USAID Tanzania.