Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) imepokea kwa Mshtuko, Simanzi na Masikitiko makubwa taarifa ya Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli usiku wa kuamkia tarehe 24.07.2020.

LEAT inatoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wote wa Serikali, Mama Anna Mkapa na familia ya Marehemu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa ujumla na inaungana na Watanzania wote katika kuomboleza msiba huu mkubwa.

Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika utetezi wa mazingira na mojawapo ya alama aliyoiacha ni Sheria ya Utunzaji wa Mazingira Namba 20 ya Mwaka 2004 ambayo ilitungwa na kupitishwa katika utawala wake. Sheria hii imechangia kwa kiwango kikubwa katika utetezi na utunzaji wa mazingira nchini Tanzania.

Kwa ujumla kama Taifa Ndugu Benjamin William Mkapa atakumbukwa pia kama kiongozi mbobezi wa diplomasia na muumini wa utandawazi aliyesimamia kwa nguvu zake zote mabadiliko makubwa katika uchumi wa Tanzania hasa katika sekta ya fedha, kudhibiti mfumuko wa bei, kukuza uwekezaji na kuboresha huduma za kijamii.

Atakumbukwa pia kwa kuasisi mipango mingi ya maendeleo na taasisi nyingi imara zinazolihudumia taifa wakati huu kama vile: Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Wakala
wa Barabara (TANROADS), Mipango ya Maendeleo ya Elimu kama vile: MMEM, MMES, MMEMKWA, mipango ya maendeleo ya afya, maji, na umeme.

Upungufu katika utendaji wake kazi na binafsi unathibitisha ubinadamu wake lakini hauwezi kudhalilisha mchango wake mkubwa alioutoa katika taifa hili ambao sisi, LEAT, tutauheshimu, kuuthamini, na kuuenzi. Kikubwa ni kuwa kama nchi lazima tusonge mbele tukienzi mazuri yote aliyoyafanya na kuyaamini na kuondoa kasoro zilizojitokeza katika utawala wake na hivyo kuwa taifa imara na lenye kuheshimu utu wa kila mtu na kuitii katiba ya nchi yetu, sheria zake, na kuiheshimu demokrasia ya kweli ambapo kila mtu ana haki ya kufurahia haki za binadamu na watu, na kulinda mazingira ya nchi yetu na kuifuata na kuitekeleza kwa makini Sheria ya Utunzaji wa Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2020.

Bwana Alitoa na Bwana Ametwaa Jina la Bwana Litukuzwe Milele yote. Amina

Bofya hapa kupata waraka uliosainiwa kutoka LEAT