Leo taifa letu linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 21 tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano yaTanzania, na Baba wa Taifa letu alipotutoka. Ni siku adhimu na inayotufanya sisi, kama taifa, kuangalia mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere katika historia ya taifa letu. Alituongoza kupigania uhuru wetu na kujenga nchi yenye misingi ya utaifa na umoja na kutuweka katika muelekeo wa kujiletea maendeleo yetu wenyewe. Aidha, alitoa mchango mkubwa sana katika kutunza Mazingira ya nchi yetu. Baba wa Taifa aliweka jitihada za kipekee kusimamia uanzishwaji wa hifadhi na alitambua umuhimu wa rasilimali za maliasili kama mtaji wa asili wa nchi.

Akiwa kama Raisi nchi ilishuhudia uanzishwaji wa hifadhi mbalimbali kama vile hifadhi ya Ruaha (1964), Mikumi (1964), Gombe (1970), Tarangire (1970) Kilimanjaro (1994), Katavi (1974), Rubondo (1977), na Mahale (1985). Uhifadhi wa maeneo haya umehakikishia Watanzania wa kizazi chake, chetu na vijavyo kuwa rasilimali hizi zitakuwepo kwa manufaa yetu sote. Aidha, alikuwa mstari wa mbele katika kutengwa kwa Agano la Kimataifa la Sheria za Bahari (United Nations Convention on the Law of the Sea (UNCLOS) ambalo lilishuhudia nchi zinazopakana na bahari kama yetu zinaongezewa ukanda wa maili mia mbili (200) kama eneo maalumu la kiuchumi (Exclusive Economic Zone)(EEZ). Aidha, Mwalimu alikuwa mstari wa mbele katika kuwahimiza wananchi kupanda miti, akisema kata mti mmoja panda miti mitatu.

Kwa kuitikia mwito wa kimataifa wa kuanzisha mamlaka za kuhifadhi mazingira Mwaka 1983 Serikali ya Tanzania ililianzisha Baraza la Utunzaji Mazingira (NEMC). Baraza lilikuja kupewa meno mnamo Mwaka 2004 pale sheria ya Utunzaji Mazingira ilipopitishwa na Bunge.

Sisi wanamazingira tunayatazama maeneo yaliyohifadhiwa kama maeneo muhimu ya kimazingira yenye kuleta utengamano wa hali ya hewa na uchumi wa wa Tanzania hasa wazalishaji wadogo waishio vijijini. Kuna mahusiano chanya tena ya moja kwa moja kati ya uwepo wa maeneo ya hifadhi na mafanikio katika sekta ya kilimo, hususani kilimo cha nchi kamaTanzania ambacho kwa kiasi kikubwa hutegemea mvua na utengamano wa hali ya hewa.

Leo, miaka 21 tangu kututoka Baba wa Taifa na takribani miaka 35 tangu kuachia kiti cha urais, tunaendelea kumkumbuka na kuishi katika nchi iliyojaaliwa maliasili ambazo yeye kama Rais alihakikisha zinalindwa kwa manufaa ya kizazi na vizazi vijavyo. Wengi wanamkumbuka kama rafiki wa haki, mkombozi wa Afrika, na mwanafalsafa wa maendeleo. Sisi LEAT tunamkumbuka kama shujaa wa kulinda maliasili na mazingira ya nchi na dunia yetu.

Kama asasi, tutaendeleza juhudi za Mwalimu Nyerere kwa kuwezesha wananchi kuelewa kuwa wao ndio msingi wa ulinzi na ufanyaji maamuzi juu ya usimamizi wa rasilimali zao.

Aidha, tunawasihi wananchi kuendelea kuishi kwa kufuata taratibu zinazoratibiwa na sheria zetu ambazo, pamoja na mambo mengine, zinawataka watu wote ndani ya Tanzania kulinda maliasili na mali ya nchi kama waamuzi wa hali ya baadae ya Taifa la Tanzania.

Heri ya Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Nyerere.

Bofya link hapa kupata waraka uliosainiwa kutoka LEAT.