LEAT INAUNGA MKONO TAMKO NA RAI YA TLS KWA UMMA JUU YA MBINU ZA KUPAMBAMBA NA UGONJWA WA KORONA

Miezi michache iliyopita, dunia imekumbana na janga kubwa la ugonjwa wa Korona ambalo limesababisha vifo vya zaidi ya watu 184,500, huku takribani watu 2,661,500 wakiwa na maambukizi ya virusi vya korona ulimwenguni kote.

Taarifa ya kusambaa kwa kirusi aina ya korona ilithibitika kuanza kusambaa katika mji wa Wuhan nchini china Mnamo Desemba 2019, kabla ya kuanza kusambaa katika nchi zingine za Ulaya na Marekani kisha barani Afrika.

Mnamo tarehe 16 Machi 2020, Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kupitia Waziri wa Afya, Jinsia na Watoto, Mh Ummy Mwalimu, ilitangaza kuingia nchini kwa ugonjwa wa virusi vya korona baada ya mgonjwa mmoja kugundulika mkoani Arusha. Hali hii ilipelekea Waziri Mkuu kuamuru kufungwa kwa shule zote za msingi hapa nchini na baada ya siku chache vyuo vyote vilifungwa kutokana na ongezeko la kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya korona.

Sambamba na hilo, Serikali ilizuia mikutano na mikusanyiko ya watu wengi katika sehemu mbalimbali isipokuwa misiba na ibada za kidini; kuzuia upakiaji wa abiria zaidi ya idadi ya viti vya kuketi katika gari; iliwataka wananchi kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, na kunawa mikono yao kwa sabuni na maji tiririka; kutumia vitakasa mikono, na kuhimiza uvaaji wa barakoa ili kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya korona.

Hadi Jumatano ya tarehe 22 Aprili 2020 wagonjwa 284 wamegundulika nchini Tanzania, huku watu 10 kati yao wakipoteza maisha. Hali ya ongezeko la idadi ya wagonjwa imeongezeka kwa kiwango kikubwa sana ndani ya mwezi mmoja.

Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira – LEAT ikiwa kama asasi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira, utetezi wa haki za binadamu kupitia kesi zenye maslahi ya umma, imekuwa ikifuatilia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa korona. Mbali na kufuatilia, imeendelea kujifunza kutoka kwa nchi zenye maambukizi makubwa namna wanavyoweka mikakati madhubuti ya kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi hivyo.

Aidha, LEAT inaunga mkono tamko na Rai ya TLS kwa umma juu ya mbinu za kupambana na ugonjwa wa korona. Tamko hili limefanywa na TLS kutokana na kutambua wajibu wao kisheria wa kuishauri serikali, Bunge, Mahakama na Umma kupitia kifungu cha 4 cha Sheria ya Chama cha Sheria (Tanganyika Law Society) cha Tanganyika, na huku wakiongozwa na Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isemayo “Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria” . Kupitia tamko hilo TLS ilitoa rai kwa umma na kupendekeza hatua mbalimbali zinazotakiwa kuchukuliwa na serikali katika kudhibiti kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa korona, huku wakitolea mfano wa nchi mbalimbali barani Afrika, Asia na Ulaya zilizoweza kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kupambana na baa hilo.

Kupitia tamko na rai iliyotolewa na TLS, LEAT inaiomba serikali kutilia maanani rai hiyo ili kuweza kulinda ustawi wa jamii ya watanzania. Aidha, inawatawaka watu wote nchini Tanzania kuendelea kuchukua tahadhari za kujilinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa korona kwa kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya. Hii ni sambamba na kukaa ndani, kunawa mikono mara kwa mara na sabuni na maji tiririka na kuepuka kukaa kwenye mikusanyiko. Katika kipindi hiki kigumu kila mtu kwa imani yake achukue nafasi ya kumuomba Mwenyezi Mungu kutunusuru na baa hili, huku tukiendelea kuchukua hatua stahiki na zenye tija katika kudhibiti na kupambana na vita hii ya janga la ugonjwa wa korona.

Bofya hapa kupata waraka uliosainiwa na TLS