LEAT PRESS RELEASES

bullet2007
bulletMar-26-2007 LEAT files Amicus Brief in Tanzanian Failed Water Privatization Case Pending Before ICSID Tribunal
bulletFeb-02-2007 LEAT, LHRC, TGNP, CIEL and IISD allowed to file written submission in Biwater v. United Republic of Tanzania ICSID arbitral dspute
bullet2004
bulletJan-10-2004 LEAT 2002-2003 Biennial Report
bullet2003
bulletNov-24-2003 Human Rights Commission Issues Injunction Order Against Tarime Gold Mine and Four Others
bulletOct-06-2003 Save Mererani Miners, Avert Another Bulyanhulu
bulletJul-29-2003 LEAT Submits Complaint to Human Rights Commission Against Afrika Mashariki Gold Mine, Tarime
bullet2002
bulletMay-17-2002 Tanzanian Attorneys Face Charges of Sedition
bulletApr-02-2002 International NGO Fact-Finding Mission on Bulyanhulu Barred from Visiting Bulyanhulu Communities
bulletJan-09-2002 Response to the National Post
bullet2001
bulletNov-26-2001 Tanzanian Police Raid LEAT Offices
bulletNov-21-2001 New assessment of controversial Commission highlights strategies to resolve contentious development projects
you are hereJul-16-2001 An Open Letter to the President of Tanzania (Kiswahili)

BARUA YA WAZI KWA RAIS BENJAMIN WILLIAM MKAPA KUHUSU UFUNGUZI RASMI WA MGODI WA DHAHABU WA BULYANHULU, KAHAMA, JULAI 18, 2001

Ndugu Rais,

Taarifa za vyombo vya habari zinaarifu kwamba unategemewa kwenda Bulyanhulu Wilaya ya Kahama kwa ajili ya kufungua rasmi Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, mali ya Shirika la Madini la Kahama (KMCL) linalomilikiwa moja kwa moja na Shirika la Dhahabu la Barrick la Canada. Taarifa mbalimbali pia zinaeleza kwamba mgodi wa Bulyanhulu ni moja ya migodi ya kisasa na yenye utajiri mkubwa wa madini duniani na ni dhahiri utaongeza kwa kiasi kikubwa mapato ya fedha za kigeni kwa wale wanaoumiliki na wenye hisa kwenye makampuni tuliyoyataja. Ni dhahiri vile vile kwamba Bulyanhulu ni jiwe linalong'ara kwenye taji la sekta ya madini Tanzania, sekta ambayo imekuwa ikikua kwa kasi kubwa hapa nchini.

Ndugu Rais,

Barua yetu haina nia ya kuelezea mafanikio tunayoambiwa yamepatikana katika sekta ya madini, na mchango wake kwa uchumi wa taifa letu ila kukumbushia na pengine kusisitizia gharama halisi za kukua kwa sekta ya madini kwa mazingira na kwa wananchi waishio kwenye maeneo yenye utajiri wa madini kama dhahabu. Hizi ni gharama ambazo zimekuwa ama hazisemwi kabisa au hazisemwi hadharani na kwa hiyo madhara yake yanaendelea kuongezeka. Wahenga wetu walisema mficha ugonjwa kilio kitamuumbua na sisi kama raia wa Tanzania tunaamini tuna wajibu wa kusema hadharani kwamba kuna ugonjwa mkubwa kwenya sekta ya madini ambao unafichwa fichwa. Bulyanhulu ni mfano bora kabisa wa mafanikio ya uwekezaji katika sekta hii na vile vile wa ugonjwa unaoikabili sekta nzima ya madini.

MCHANGO WA WANANCHI WA BULYANHULU

Ndugu Rais,

Machimbo ya dhahabu ya Bulyanhulu hayakugunduliwa na wawekezaji wala na wataalamu wa Serikali bali yaligunduliwa na wananchi wa kawaida waliokuwa wanajishughulisha na uchimbaji mdogo mdogo wa madini hayo. Kati ya mwaka 1975 yalipogunduliwa machimbo hayo hadi mwaka 1990 wachimbaji wadogo wadogo waliendelea kuchimba dhahabu katika eneo hili, lakini kwa vile Serikali ilikuwa haitambui rasmi shughuli hizi, dhahabu, kama yalivyokuwa madini mengine ya thamani, iliendelea kutoroshwa na walanguzi kupitia nchi jirani.

Ndugu Rais,

Hali hii ya dhahabu ya Bulyanhulu kunufaisha nchi jirani ilibadilika ghafla kuanzia mwezi Aprili, 1990, wakati Serikali ya Awamu ya Pili, ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, ilipoamua rasmi kwamba Serikali kwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania ianze kununua dhahabu ya wachimbaji wadogo wadogo kwa bei za soko huria na bila kuwabughudhi wananchi. Matokeo ya uamuzi yalijoinyesha mara moja: kujitokeza mara moja. Ndugu Rais, takwimu za Halmashauri Kuu ya chama chako mwenyewe, yaani Chama cha Mapinduzi zinaonyesha kwamba kati ya mwaka 1991 hadi 1996, dhahabu ya wachimbaji wadogo wadogo ilileta shilingi bilioni 8.5 (1991), shilingi bilioni 12.2 (1992); shilingi bilioni 13.04 (1993); shilingi bilioni 12.4 (1994); shilingi bilioni 1.9 (1995) na shilingi bilioni 1.6 (1996). (Angalia, "Chama cha Mapinduzi: Tathmini ya Miaka Ishirini ya CCM, 1977-1997", Halmashauri Kuu ya Taifa, 1998).

Takwimu za Benki ya Dunia kwa kipindi hicho zinaonyesha kwamba thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola moja ya Marekani zilikuwa kama ifuatavyo: Shilingi 219 (1991); shilingi 298 (1992); shilingi 405 (1993); shilingi 510 (1994); shilingi 575 (1995) na shilingi 580 (1996). Kwa kutumia takwimu hizi, dhahabu ya wachimbaji wadogo wadogo ililiingizia Taifa mapato ya fedha za kigeni kama ifuatavyo: Dola za Marekani milioni 38.89 (1991); milioni 40.91 (1992); milioni 32.2 (1993); milioni 24.3 (1994); milioni 3.3 (1995) na milioni 2.76 (1996). Takwimu za Wizara ya Madini na Nishati vile vile zinaonyesha mapato ya fedha za kigeni ya dola za Marekani milioni 13.64 mwaka 1990, mwaka ambao sera ya Serikali ya kununua dhahabu kwa wachimabaji wadogo wadogo ilianza kufanya kazi rasmi.

Ndugu Rais,

Huu ulikuwa ni mchango mkubwa sana wa wachimbaji wadogo wadogo kwa uchumi wa Taifa letu kama ambavyo tathmini ya miaka 20 Chama cha Mapinduzi inavyokiri katika ibara ya 102. Ndio maana katika Programu ya Chama cha Mapinduzi iliyotolewa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama chako mwaka 1992, iliahidi kwamba

"Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuhimiza kuwekwa kwa utaratibu mzuri ili wananchi waweze kushiriki katika uchimbaji wa madini bila kuathiri mazingira…. Aidha, hatua ambazo zimekwishachukuliwa za kuwawezesha wachimbaji wadogo kuuza dhahabu na almasi benki kuu zitaendelezwa maana faida zake kwa nchi zimejitokeza wazi wazi." (Programu ya Chama cha Mapinduzi: Mwelekeo wa Sera Katika Miaka ya Tisini, ibara ya 61).

Kwa kiasi kikubwa, mchango huu mkubwa kwa uchumi wa Taifa ulitokana na wachimbaji wadogo wadogo wa Bulyanhulu kwa sababu machimbo ya Bulyanhulu ndiyo yalikuwa machimbo tajiri sana kwa dhahabu kuliko machimbo mengine hapa nchini. Ni wazi vile vile kwamba wachimbaji wadogo wadogo walichangia kwa kiasi kikubwa sana kuinua hali ya kiuchumi ya maeneo yao na vile vile ya Wilaya ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga. Wamilikaji wa sasa wa machimbo hayo yaani Shirika la Madini la Kahama wanakiri wenyewe kuhusu jambo hili. Hivi ndivyo walivyosema kwenye ripoti za mradi walizopeleka Benki ya Dunia kuombea mkopo wa kuendeleza machimbo ya Bulyanhulu:

"Ijapokuwa hakuna takwimu sahihi zilizowekwa, mara baada ya ziara ya Rais Ali Hassan Mwinyi Bulyanhulu mwaka 1994, kulikuwa na ongezeko kubwa la wachimbaji wadogo wadogo katika machimbo ya Bulyanhulu la kati ya watu 30,000 hadi 400,000…. Shughuli za uchimbaji mdogo mdogo wa dhahabu zilileta matokeo mazuri kwa kuongeza vipato vya familia, kuongeza vyanzo vya mapato, kupanua ajira na kuboresha huduma za jamii kama usafiri na biashara."

Ripoti hizo zinaendelea kueleza kuwa:

"inaaminika eneo hili lilikuwa na viwango vikubwa sana vya vipato kupita sehemu nyingine yoyote katika Mkoa wa Shinyanga."

Na kwamba wachimbaji wadogo wadogo wa Bulyanhulu walichangia maendeleo ya Bulyanhulu:

"kwa kulipa kodi na michango mbali mbali ilitumika kuendeleza huduma za jamii kama vile kujenga madarasa mawili ya Shule ya Msingi ya Kakola."

Kuingia kwa Wawekezaji wa KMCL

Ndugu Rais,

Mambo tuliyataja hapo juu yalianza kubadilika ghafla mnamo mwaka 1994 wakati Wizara ya Madini na Nishati ilipoamua kugawa eneo la Bulyanhulu kwa wawekezaji kutoka nje. Kwanza uamuzi wenyewe unaonekana kuwa ulitolewa kimizengwe kwa sababu ushahidi wa kimaandishi kutoka Wizara hiyo unaonyesha wazi wazi kwamba Shirika la Madini la Kahama halikuwahi kupewa leseni ya kutafiti madini katika eneo la Bulyanhulu wala katika eneo lingine lolote katika Wilaya nzima ya Kahama. Ushahidi huu unaonyesha kwamba mkataba wa kuwapa wawekezaji wa KMCL leseni ya miaka mitatu ya kutafiti madini ya dhahabu uliosainiwa na Waziri wa Madini na Nishati wa wakati huo, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mnamo tarehe 6 Septemba 1994, ulikuwa unahusu "eneo la Butobela, Wilaya ya Geita." Nyongeza mbili za muda wa leseni hiyo zilitolewa na Kamishna wa Madini tarehe 24 Julai 1997 na tarehe 6 Oktoba 1998 vile vile zinaonyesha kwamba leseni hiyo Namba 216 ya 1994 ilitolewa kwa ajili ya eneo la Butobela, wilayani Geita. Vile vile orodha ya Wizara ya Madini na Nishati ya maeneo yote yaliyotolewa leseni za kutafiti madini inaonyesha kwamba leseni namba 145 ya 1994 inayohusu eneo la Bulyanhulu ilitolewa kwa Kampuni ya Madini ya Afrika Mashariki, yaani East Africa Mines Ltd. na wala sio KMCL.

Ndugu Rais,

Licha ya kwamba KMCL haikuwa na leseni ya kutafuta madini ya dhahabu eneo la Bulyanhulu, kampuni hiyo ilianza hujuma na vita dhidi ya wachimbaji wadogo wadogo wa Bulyanhulu mara moja. Katika hujuma na vita hii, KMCL ilisaidiwa na viongozi waandamizi wa Wizara ya Madini na Nishati. Kwa mfano kumbukumbu za maandishi zilizoko Wizara hiyo zinaonyesha kwamba katika kikao kati ya wajumbe wa wachimbaji wadogo wadogo wa Bulyanhulu na Naibu Waziri wa Maji, Madini na Nishati wa wakati huo, Mheshimiwa Profesa Joseph Mbwiliza kilichofanyika Makao Makuu ya CCM Dodoma, tarehe 30 Aprili, 1995, Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Ndugu Stephano Mashishanga alimuomba Naibu Waziri awahakikishie wajumbe wa wachimbaji wadogo wadogo nia ya Serikali kuwepo kwao katika machimbo ya Bulyanhulu. Kumbu kumbu za kikao hicho zinaonyesha kwamba Naibu Waziri:

"alikubaliana na maombi ya wajumbe na kutamka wazi kuwa anawahakikishia viongozi wa kijiji pamoja na wachimbaji wote waendelee na uchimbaji katika eneo wanalochimba hadi sasa bila bughudha. Wizara yake inafanya majadiliano na kampuni ya Kahama Mining Corporation Ltd. iliyoko Bulyanhulu ili kupata ufumbuzi wa mwafaka kwa pande zote zinazohusika."

Kumbu kumbu hizi zilisainiwa na Naibu Waziri mwenyewe ambaye ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho. Hata hivyo wiki mbili tu baadaye Naibu Waziri huyo huyo alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akikanusha kwamba Serikali iliruhusu wachimbaji wadogo wadogo Bulyanhulu! (Angalia matoleo ya magazeti ya Majira, Jumamosi, Mei 13, 1995; na Daily News, Jumatatu, Mei 15, 1995).

Ndugu Rais,

Matokeo ya msimamo huu wa Serikali ilikuwa ni kuipa kichwa KMCL ambao iliamua kufungua kesi dhidi ya wachimbaji wadogo wadogo wa Bulyanhulu mwezi mmoja baadaye, yaani Juni 1995 ikiiomba Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na mambo mengine, itoe amri ya kuwaondoa wachimbaji wadogo wadogo katika maeneo ya machimbo ya Bulyanhulu na ya kuwazuia wasifanye tena shughuli za uchimbaji katika eneo hilo. Kwa vile KMCL ilikuwa inataka kuwaondoa wachimbaji wadogo wadogo bila ya kuwalipa fidia yoyote kwa mali na vitega uchumi mbali mbali walivyokuwa navyo wananchi hawa, kitu ambacho ni kinyume cha misingi ya haki za binadamu iliyoko kwenye Katiba ya nchi yetu, mnamo tarehe 29 Septemba 1995, Mahakama Kuu ya Tanzania iliamuru kwamba kesi hiyo isikilizwe na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu kama inavyotakiwa na sheria za nchi yetu.

Mnamo tarehe 5 Oktoba 1995, KMCL iliamua kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa Mahakama Kuu katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. Hata hivyo kwa sababu ambazo hazijulikani hadi hivi leo, KMCL kwa kupitia mawakili wao, iliamua kuondoa rufaa yao Mahakama ya Rufaa mnamo tarehe 22 Mei, 1996 na kubakisha kesi iliyokuwa imeifungua Mahakama Kuu. Kile kinachojulikana ni kwamba mara baada ya KMCL kuondoa rufaa yao, vyombo vya habari vilianza kutangaza kwamba Serikali ilikuwa imeamua kuwaondoa wachimbaji wadogo wadogo wa Bulyanhulu licha ya kesi iliyokuwa imefunguliwa dhidi yao kuwepo bado Mahakama Kuu ya Tanzania. (Angalia toleo la gazeti la East African lenye kichwa cha habari "Company to Evict 7,000 Illegal Miners" likimkariri aliyekuwa Waziri wa Madini na Nishati wakati huo, Dr. William Shija akisema kwamba wachimbaji wadogo wadogo wangeondolewa kwa nguvu kutoka eneo la machimbo kati ya miezi ya Julai na Agosti ya mwaka huo).

Tuhuma za Mauaji Bulyanhulu

Ndugu Rais,

Mnamo tarehe 30 Julai 1996, Waziri Shija aliitisha mkutano wa waandishi kwenye Ukumbi wa Bunge Dodoma ambako alitoa amri kwa wachimbaji wadogo wadogo wa Bulyanhulu kuondoka wenyewe kwenye maeneo ya machimbo haya katika kipindi cha mwezi mmoja! (Angalia matoleo ya magazeti ya Daily News ya Jumatano, Julai 31, 1996 yenye kichwa "Government orders out Bulyanhulu miners"; na Mtanzania ya Jumatano, Julai 31, 1996 yenye kichwa cha habari "Serikali yaamuru walioko machimboni Bulyanhulu wahame"). Mchana wa siku hiyo hiyo na mara tu baada ya Radio Tanzania kutangaza amri hiyo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Meja Jenerali Tumainieli Kiwelu, aliitisha mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kakola ambapo alipunguza muda uliotolewa na Waziri Shija wa wachimbaji wadogo wadogo kuondoka Bulyanhulu kuwa siku saba na shughuli za uchimbaji kusimamishwa ndani ya Saa 12! Usiku huo huo idadi ya polisi zaidi ya 60 walipelekwa katika maeneo ya machimbo tayari kuanza kuwaondoa wachimbaji wadogo wadogo kwa nguvu. (Angalia toleo la gazeti la The Guardian la tarehe 9 Septemba, 1996, lenye kichwa cha habari "The day hell broke loose at Bulyanhulu").

Ndugu Rais,

Kwa kuwa KMCL ilikuwa bado na kesi dhidi ya wachimbaji wadogo wadogo katika Mahakama Kuu ya Tanzania, wachimbaji waliamua kukimbilia Mahakama Kuu ili kuiomba kuingilia kati suala la kuondolewa kwao kinyume cha taratibu na sheria za nchi yetu. Mnamo tarehe 2 Agosti 1996, Mahakama Kuu ya Tanzania, Tabora ilitoa amri ya kizuizi dhidi ya KMCL na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kuwazuia kuendelea na zoezi la kuwaondoa kwa nguvu wachimbaji wadogo wadogo, zoezi ambalo lilikuwa limeingia siku yake ya tatu. Uamuzi huu wa Mahakama Kuu ulitangazwa na Radio Tanzania usiku wa siku hiyo hiyo na baadaye kupelekwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Meja Jenerali Kiwelu na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Charles Mnubi waliokuwa wanasimamia operesheni hiyo ya kuwaondoa wachimbaji wadogo wadogo.

Amri ya Mahakama Kuu haikufuatwa wala kuheshimiwa na watendaji hawa. Matokeo yake, siku chache baadaye, vyombo vya habari vilitangaza kutokea mauaji makubwa ya wachimbaji wadogo wadogo Bulyanhulu ambao inadaiwa walifukiwa hai ndani ya mashimo ya migodi. (Angalia matoleo ya magazeti ya Majira, Jumatatu, Agosti 12, 1996 - "Kufuatia amri ya kuwatimua wachimbaji wadogo: Watu 23 wahofiwa kufunikwa na 'greda' Bulyankulu"; na Mtanzania, Jumanne, Agosti 13, 1996 - Utata Watawala Maafa ya Kahama: Waliokufa machimboni wahofiwa kufikia 52: Picha za maiti zapelekwa Dodoma, wadaiwa kufunikwa na magreda"). Taarifa hizi pia zilitoa majina ya waliohofiwa kufa na kuongeza kwamba polisi walikuwa wanazuia wananchi kusogelea maeneo walikofia ndugu na jamaa zao kiasi kwamba baadhi ya maiti za watu waliofukuliwa ziliachwa zinaoza nje bila kuzikwa. Vile vile kulikuwa na taarifa za walionusurika na janga hilo ambao walitoa maelezo kwa vyombo vya habari. (Angalia toleo la Majira, Ijumaa, Agosti 30, 1996 - "Aliyenusurika kufukiwa Bulyanhulu ataja waliokufa: Adai wenzake wanne wamekufa").

Baadaye vyombo vya habari vilitangaza kwamba polisi waliokuwa katika maeneo ya machimbo walikuwa wanazuia wananchi kufukua maiti pale ilipojitokeza kwamba kweli wachimbaji wadogo wengi walikuwa wameuawa ndani ya machimbo hayo. (Angalia Majira, Jumanne, Agosti 20, 1996 - "Ufukuaji wa maiti Bulyankulu wakwama"). Juhudi za kujitolea za wananchi wenyewe kuwafukua ndugu na jamaa zao vile vile zilizuiliwa na polisi. (Angalia Majira, Jumapili, Agosti 25, 1995 - "Wachimbaji wajitolea kufukua mashimo Bulyankulu"; Mtanzania, Ijumaa, Septemba 13, 1996 - "Wadai watu wamefukiwa Bulyankulu"; na The Guardian, Jumatatu, Septemba 9, 1996 - "The day hell broke loose at Bulyankulu"). Ilichukua zaidi ya mwezi mzima kwa wale wanaotuhumiwa kuhusika moja moja na mauaji haya kukanusha hadharani habari za mauaji haya! (Angalia Majira ya tarehe 17 Septemba, 1996 - Hakuna waliofukiwa mashimoni Bulyankulu - Kiwelu"). Taarifa hiyo ilimkariri Jenerali Kiwelu akiwaita watu waliokuwa wanadai mauaji yametokea kuwa ni "waongo na wazushi."

Ndugu Rais,

Taarifa za mauaji ya wachimbaji wadogo wadogo hatimaye zilivifikia vyombo vya kutetea haki za binadamu kama Amnesty International ambayo kwa miaka minne mfululizo (1997-2000) imekuwa ikichapisha habari hizo na kuitaka Serikali kuunda tume huru ya uchunguzi wa mauaji haya. Hata hivyo Serikali imekuwa ikikataa kufanya hivyo kwa madai hayo hayo ya Jenerali Kiwelu kwamba hakuna watu waliokufa. Hata hivyo Serikali haijawahi kutoa taarifa ni kwa jinsi gani watu zaidi ya lake nne, waliokuwa kwenye machimbo hayo, waliovyondoka katika kipindi cha siku saba zilitolewa na Jenerali Kiwelu. Vile vile Serikali haijawahi kueleza ni kwa nini polisi wengi hivyo walipelekwa Bulyankulu usiku wa tarehe 30 Julai 1996 wala sababu zilizoifanya Serikali kupuuza amri halali ya Mahakama Kuu ya Tanzania ya kuzuia kuondolewa kwa nguvu kwa wachimbaji wadogo wakati kesi iliyofunguliwa dhidi yao na KMCL ikiwa bado mahakamani. Ni wazi kwamba watu kama Jenerali Kiwelu na maafisa waandamizi wa polisi wasingeaminika na mtu yeyote kuwa watasema ukweli kwani wao wenyewe walikuwa wanatuhumiwa kushiriki moja moja kwenye maafa hayo.

Licha ya taarifa za maafa haya makubwa, wachimbaji wadogo wadogo wa Bulyanhulu pia waliharibiwa mali zao na vitega uchumi vyao kuangamizwa bila ya malipo yoyote ya fidia, kinyume kabisa na sheria na taratibu za nchi hii. Nyumba zaidi ya 3,000 zinasemekana zilivunjwa wakati wa operesheni ya kuwaondoa wachimbaji wadogo. Mashamba yaliharibiwa na mali zingine kupotea. Matokeo ya uharibifu huu ni kwamba hali ya kiuchumi na kijamii ya wananchi wa Bulyanhulu imekuwa mbaya sana. Hata wawekezaji wenyewe wanalikubali hili. Katika ripoti yao kwa Benki ya Dunia, KMCL wanakiri kwamba:

"kufungwa kwa shughuli za uchimbaji mdogo mdogo kulikuwa na matokeo mabaya sana kwa shughuli za kiuchumi, kwa idadi ya watu na kwa maendeleo ya jamii, matokeo ambayo athari zake zimesambaa mbali zaidi ya eneo lenyewe la machimbo"!

Ripoti hiyo inaongeza kwamba:

"inaaminika kwamba kabla ya kufungwa kwa machimbo ya wachimbaji wadogo wadogo, wastani wa mapato katika eneo hili ulikuwa ni wa juu zaidi katika mkoa wa Shinyanga. Mapato haya yameshuka tangu kufungwa kwa machimbo ya wachimbaji wadogo wadogo."

Haya ni maneno ya wawekezaji wenyewe na ambayo hayawezi kuitwa ya "uongo au uzushi"!

Maombi Yetu Kwako

Ndugu Rais,

Barrick Gold Corporation inajulikana kuwa ni kampuni ya dhahabu tajiri kuliko nyingine zote duniani. KMCL na wamilikaji wao Barrick wenyewe wamesema kwamba Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu ni mmoja wa migodi tajiri sana kwa dhahabu duniani na ni wa pili kwa utajiri kwa migodi wanayomiliki sehemu mbali mbali za Amerika ya Kaskazini na ya Kusini. Barrick wanajitapa kwamba Bulyanhulu ni mradi wenye gharama ndogo zaidi kuliko miradi yao yote! Haya ni maneno ya Rais na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Bwana Randall Oliphant kwenye mkutano wa wenye hisa wa kampuni uliofanyika Toronto, Canada tarehe 8 Mei mwaka huu wa 2001. Hata kama maneno haya yangekuwa ni ya majigambo tu, hatungetakiwa kuyapuuzia.

Kwa bahati mbaya, Ndugu Rais, maneno haya si majigambo hata kidogo bali ni ukweli mtupu. Kwa nini?

Kwanza, KMCL na wamilikaji wao waliupata mgodi bila kutakiwa kulipa fidia yoyote kwa mamia ya maelfu ya wananchi wachimbaji wadogo ambao KMCL wenyewe inadai waliruhusiwa kuendesha shughuli zao na Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi. Hii ina maana kwamba waliupata huu mgodi bila gharama yoyote au kwa gharama ndogo sana. Pili, KMCL na wamilikaji wenzao watauendesha Mgodi wa Bulyanhulu kwa gharama ndogo sana. Kwani kufuatana na taarifa ya Benki ya Dunia ambayo inaudhamini Mgodi huo, Serikali ya Tanzania inatazamiwa kupata jumla ya dola za Marekani milioni 75 kama kodi na ushuru mwingine katika kipindi cha miaka 15 ya Mgodi huo. Hii ni sawa na dola milioni 5 kwa mwaka! Wamilikaji wa mradi wenyewe wanasema kwamba mapato yao katika kipindi hicho kutokana na mradi yatafikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 3 au mara 40 ya kile wanachotarajia kutupatia sisi kama Taifa! Kama tulivyoonyesha mwanzoni, miaka kumi iliyopita, Taifa letu lilikuwa likipata fedha nyingi zaidi za kigeni kutokana na wachimbaji wadogo wadogo. Ni wazi huu sio uwekezaji wa kutusaidia bali ni wa kupora rasilmali ya taifa, kutuangamiza, na kutufanya kuwa maskini daima dumu.Na kibaya zaidi utakkifanya kizazi hiki cha Watanzania kutosamehewa kamwe na vizazi vijavyo kwa kuruhusu mali asili ya nchi hii kupora wakati kikiwa na uwezo wa kukataa hayo kutokea.

Ndugu Rais,

Ombi letu kwako ni kwamba uingilie kati masuala haya na kufanya, pamoja na mambo mengine, yafuatayo:

  1. Kuhakikisha kwamba tume huru ya uchunguzi inaundwa kuchunguza kwa kina matukio ya mwaka 1996 ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka, mioyo ya watu waliopoteza ndugu na jamaa zao inaridhika na mizimu ya waliopoteza maisha yao inatulizwa kwa kupatiwa maziko ya heshima yanayofaa binadamu. Tume hii iundwe na ijumuishe watu waadilifu na wanaoheshimika na Taifa kwa utashi na busara zao. Kuundwa kwa tume hii na kufanyika kwa uchunguzi huru, kina na kImo utawaondolea wananchi wengi ndani ya nchi yetu na nchi za nje hisia zinazojengeka na kukua kwa kasi kwamba awamu hii ya urais imejaa visa na matukio mengi ya mauaji ya wananchi, na huku serikali yako ikikataa, kwa makusudi kabisa, kuchukua hatua zozote dhidi ya wanaotuhumiwa kuhusika na matukio haya. Tunaamini kuwa Tume ya namna hii vile vile itathibitisha wazi wazi kwamba utawala wako ni wa uadilifu, wa ukweli na wa uwazi zaidi ya yote unaheshimu Katiba na Sheria za nchi yetu pamoja na maisha ya Watanzania na si ya wachachetu na wenye nasaba nzuri.

  2. Kuhakikisha kwamba wananchi wa Bulyanhulu walioathiriwa na wanaoendelea kuathirika na mradi huu, ama kwa kupoteza ndugu au jamaa zao au kuharibiwa mali na vitega uchumi vyao, wanalipwa fidia zote zinazotakiwa kisheria. Hili ni jambo linalowezekana. Kama tulivyosema, KMCL na wamilikaji wao Barrick Gold Corporation ni moja ya makampuni tajiri ya dhahabu duniani na wao wenyewe wanajigamba kwamba wameupata Mgodi wa Bulyanhulu kwa bei sawa na bure!. Vile vile wao wenyewe wanakiri kwamba kuwepo kwao Bulyanhulu kumesababisha kushuka kwa hali za maisha za wananchi wa eneo hili. Haki vile vile inadai kwamba wananchi hawa nao watendewe haki.

  3. Hatua za dhati zichukuliwe kuwawajibisha wale wote wanaojulikana na watakaojulikana kuhusika moja kwa moja na mauaji ya wananchi na kudharau amri halali ya Mahakama Kuu ya Tanzania. Wewe mwenyewe Ndugu Rais wakati ya maadhimisho ya Sherehe za Mei Mosi, mwaka huu, uliwataka wananchi wasiwe wanajichukulia sheria mikononi mwao kupambana na uhalifu bali wawapeleke watuhumiwa wa uhalifu kwenye vyombo vya sheria. Iweje basi wale waliodharau amri halali ya vyombo vya sheria kuhusiana na suala la Bulyanhulu wameachwa kuendelea na nyadhifa zao bila kutakiwa kuwajibika mbele ya umma na mbele ya sheria?

  4. Kuhakikisha kwamba kweli Taifa letu linafaidika na rasilmali tuliyo nayo. Hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba mkataba kati ya Serikali na KMCL na wamilikaji wao unaangaliwa upya kwa lengo la kuongeza kiwango cha mapato kwa Taifa. Wakati Barrick Gold Corporation walipoichukua KMCL mwaka 1999 waliiambia Serikali kwamba eneo la Bulyanhulu lilikuwa na utajiri wa dhahabu wa kiasi cha aunsi milioni 3.6 zilizothibitishwa. Kufikia mwisho wa mwaka jana walikuwa wanasema utajiri huo umeongezeka kufikia aunsi milioni 7.5 zilizothibitishwa. Na miezi miwili iliyopita Rais na Mtendaji wao Mkuu amesema kwamba Buly (kama wanavyoiita Bulyanhulu!) ina utajiri uliothibitishwa wa aunsi milioni 10.5 na zinaendelea kuongezeka. Ni wazi hawa wawekezaji hawakuieleza Serikali ukweli wote juu ya utajiri wa eneo hili. Na hata kama na wao hawakujua, ni wazi kwamba hali halisi imebadilika kwa namna ambayo haikutegemewa wakati Serikali inakubali kuwa itakuwa inapokea dola za Marekani milioni tano kwa mwaka. Hii inapotokea sheria za mikataba zinakubali kwamba mkataba unaweza kuvunjwa au kujadiliwa upya. Kwa hiyo hili nalo linawezekana kisheria na kiuchumi vile vile kwa kuzingatia haya tuliyoyasema.

Ndugu Rais,

Kufanyika mambo haya kutaudhihirishia umma wa Watanzania kwamba Serikali ya Awamu ya Tatu sio Serikali inayofumbia macho matukio machafu ya ukiukaji wa haki za binadamu za wananchi na sio Serikali iliyotekwa nyara na wawekezaji wa nje ili kurahisisha uporaji wa rasilmali za Taifa letu. Vile vile kutaondoa hisia za watu wengi, ndani na nje ya nchi yetu, kwamba Serikali ya Awamu ya Tatu imetawaliwa na vitendo ambavyo Watanzania hatukuwahi kuvishuhudia katika karibu miaka ishirini na mitano ya Awamu ya Kwanza ya Marehemu Mwalimu Nyerere na miaka kumi ya Awamu ya Pili ya Mzee Mwinyi. Tuna imani utaliangalia suala hili kwa makini na kulipa uzito unaotakiwa. Barua hii kwako imeandikwa nasi tukitumia haki yetu ya kikatiba kama ilivyotolewa na ibara ya 18 kuhusu uhuru wa kutoa maoni, ibara ya 26 inayotaka kila raia wa nchi yetu kuhakikisha kuwa sheria za nchi yetu zinaheshimiwa na kufuatwa, na ibara ya 27 ambayo inamtaka kila raia wa nchi yetu kuhakikisha kuwa mali asili na utajiri wa nchi yetu unatumiwa vizuri. Ibara ya 27 inasema:

27(1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine;

(2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.(Mkazo ni wetu)

Jukumu hili ni kubwa na, kwetu sisi ni takatifu, ambalo linatakiwa kutekelezwa bila haya wala kujivutavuta na kila Mtanzania ambaye anaitakia mema nchi yetu pamoja na kizazi kijacho cha Watanzania. Inatia uchungu sana kuona kuwa baada ya Watanzania wengi kwenda shule na kupata elimu bado nchi yetu inakubali kuingia mikataba ya Shanga, kama ile ya Chifu Mangungo na Karl Peters, na wanyonyaji ambao si tu wanaharibu mazingira yetu na kutuachia mashimo matupu, bali pia wanashiriki katika kuua watu wetu. Je, hivi ni kweli tumekuwa wavivu wa kutumia akili zetu kuhakikisha kuwa utajiri wa nchi yetu hauporwi na Watanzania wasigeuke kuwa watumwa katika nchi yao? Uvivu huu, umeanza lini?

Ulipoapishwa kuwa Rais wa nchi yetu mnamo Mwaka 1995 na 2000 uliapa kuwa "utaitii, kuiheshimu na kuitetea Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na sheria zote za nchi zilizotungwa kwa mujibu wa katiba", Ndugu Rais, hatutaki kuamini kuwa umeshindwa kutekeleza kiapo hicho bali utafuatilia kwa makini na haraka haya yote tuliyoyaeleza katika barua hii kwa nia njema ili kuhakikisha kuwa mali asili ya nchi yetu inatumiwa vizuri kwa manufaa ya Watanzania na si ya wanyonyaji kutoka nje.

Ndugu Rais tunakutakia nguvu, hekima, busara na ushujaa wa kufuatilia suala hili na tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwako.

Lawyers' Environmental Action Team (LEAT)

Rugemeleza Nshala
Rais-LEAT